Acts 6

Mateso Na Kuenea Kwa Injili

(6:1–9:31)

Saba Wachaguliwa Kuhudumu

1 aBasi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 bWale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 cKwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 dnasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”

5 eYale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 fWakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.

7 gNeno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

Kukamatwa Kwa Stefano

8 hStefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. 9 iHata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 jLakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.

11 kNdipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.”

Stefano Afikishwa Mbele Ya Baraza

12 lWakawachochea watu, wazee na walimu wa Torati, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza. 13 mWakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Torati. 14 nKwa maana tumemsikia akisema kwamba Isa Al-Nasiri atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Musa.”

15 oWatu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang’aa kama uso wa malaika.
Copyright information for SwhKC